Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akizungumza na Mwakilishi Mkuu wa Shirika l...

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akizungumza na
Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA)
nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase kuhusu Japan na Tanzania kushirikiana
katika masula ya TEHAMA . Bw. Toshio Nagase amekutana na kufanya
mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Faustin Kamuzora leo jijini Dar es salaam.

Mwakilishi Mkuu wa Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase
akimweleza jambo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto).

Mwakilishi Mkuu wa Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase
(kulia) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo upande wa
Mawasiliano wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora.

Mwakilishi Mkuu wa Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase
(kulia) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo upande wa
Mawasiliano wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akisisitiza
jambo alipokutana na Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase. Bw. Toshio
Nagase amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
kuhusu namna Japan na Tanzania zinavyoweza kushirikiana katika masula ya
TEHAMA .Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
--
Na. Aron Msigwa –MAELEZO
Dar es salaam.
Tanzania na Japan zinatarajia
kuanzisha ushirikiano katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwaunganisha wafanyabishara na vijana
wanaojihusisha na masuala ya TEHAMA ili waweze kunufaika na fursa
zilizopo katika nchi hizo.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar
es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Faustin Kamuzora mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na
Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA)
nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase ambaye alimtembelea ofisini kwake
kueleza nia ya Shirika lake na nchi ya Japan kutaka kuwekeza kwenye
Sekta ya TEHAMA nchini Tanzania.
Amesema mara baada ya kukamilika
kwa taratibu zote za ushirikiano katika sekta ya TEHAMA vijana na
wafanyabishara wa Tanzania wataweza kushirikiana na vijana na
wafanyabiashara kutoka Japan katika kubadilishana uzoefu na ujuzi katika
masuala ya TEHAMA na kuwawezesha kujiajiri wenyewe au kuajiriwa ndani
na nje ya nchi.
Prof. Kamuzora amesema kuwa
Tanzania na Japan kwa muda mrefu zimekuwa zikishirikiana katika masuala
mbalimbali ya maendeleo kupitia miradi ya ushirikiano hususan ujenzi wa
miundombinu na masuala ya Ufundi.
Aidha, amesema kuwa Tanzania
imekuwa ni nchi ya kuigwa duniani na kupigiwa mfano kwa kuwawezesha
wananchi kupata huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia simu za mkononi
na kufanya malipo mbalimbali.
“sisi kama Serikali
tunawakaribisha wenzetu wa Japan kuja Tanzania kushirikiana nasi
kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na kuwekeza nchini kwetu ili wananchi
wetu wanufaike na maendeleo ya Sekta hii kama ambavyo wenzetu wamepiga
hatua kwa kuwa na kampuni za vifaa vya TEHAMA kama vile kampuni ya
Sony”. Amesema Prof. Kamuzora.
Amesisitiza kuwa Serikali ya
awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli imeweka msisitizo
katika uanzishaji na uendelezaji wa viwanda kwa lengo la kukuza ajira
miongoni mwa watanzania na kuongeza kuwa mkakati uliopo ni kuanzisha
viwanda vya kuzalisha vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa kuwa Soko bidhaa
hizo lipo.
Ameongeza kuwa Serikali ya
Tanzania kwa kushirikiana na JICA imejipanga kuwekeza katika Elimu,Ujuzi
na Stadi kwa vijana ili waweze kutengeneza Program za TEHAMA ambazo
zinahitajika ndani na nje ya nchi hivyo kukuza uchumi miongoni mwa
vijana hao.
Kuhusu kuwekeza katika Elimu
katika masuala ya TEHAMA Prof. Kamuzora amesisitiza kuwa hakuna nchi
iliyowahi kuendelea duniani bila kuwa na wabunifu wake wa ndani na
kuongeza kuwa Tanzania sasa inao vijana wenye uwezo wanaofanya vizuri
katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
“Dhana ya kutengeneza viwanda
lazima ihusishe ubunifu wa kutengeneza Programu, hakuna nchi
iliyoendelea bila kuwa na wabunifu wa ndani tunachohitaji sasa ni uwepo
wa vijana ambao wakao tayari ” Amesisitiza Prof. Kamuzora.
Prof. Kamuzora amesema Tanzania
inazo fursa nyingi za kuwawezesha vijana ikiwemo uanzishaji wa viwanda
vidogo na vya kati vya kutengeneza programu za TEHAMA hivyo ushirikiano
ulioonyeshwa na JICA utawezesha viwanda vya kutengeneza vifaa
mbalimbali kuanzishwa kupitia wabunifu waliopo.
“ Tanzania tunao vijana wabunifu
wenye uwezo, kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) wameweza
kubuni na kutengeneza teknolojia mbalimbali kusaidia shughuli za Kilimo
na uhifadhi wa Maliasili hapa nchini” Amesema.
Aidha, amesema Wizara kwa
kushirikiana na JICA inafanya mpango wa kuwakutanishawafanyabiashara;
wawekezaji; kampuni; sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Sekta ya
Mawasiliano wa Tanzania na Japan ili kubadilishana uzoefu na kuainisha
fursa na maeneo ya kushirikiana kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo na
ushirikiano wa nchi hizo mbili kwenye Nyanja ya TEHAMA.
Kwa upande wake mwakilishi Mkuu
wa JICA nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase akizungumza mara baada ya
kufanyika kwa mazungumzo hayo amesema kuwa Tanzania na Japan kwa miaka
mingi zimekuwa na ushirikiano wa karibu katika masuala mbalimbali.
Ameipongeza Tanzania kwa kupiga
hatua na kufanya vizuri katika matumizi ya TEHAMA kwenye huduma za fedha
kwa njia ya Simu na kubainisha kuwa Japan inayo mengi ya kujifunza
kupitia mafanikio haya.
Amesma JICA imejipanga kusaidia
awamu ya pili ya program zao nchini Tanzania hususan kwenye Miundombinu,
uwekezaji kwenye TEHAMA na masuala ya kiufundi katika maeneo mbalimbali
ambayo miradi ya ushirikiano inatekelezwa.
Nagase ameeleza kuwa Japan
imejipanga kushirikiana kikamilifu katika masuala ya TEHAMA hususan
kuwawezesha vijana na wafanyabiashara wa Tanzania na Japan kubadilishana
uzoefu, ujuzi, ufundi katika masuala ya TEHAMA.
Amebainisha kuwa Japan iko tayari
kushirikiana na Sekta binafsi nchini Tanzania kupitia biashara na
uwekezaji kwenye makampuni yanayojishughulisha na TEHAMA.