Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Richard Kasuga akitoa ufafanuzi leo jijin...

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Richard
Kasuga akitoa ufafanuzi leo jijini Dar es Salaam kuhusu mgawanyo wa
pembejeo za kilimo kwa wakulima nchini kote. Kulia ni Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Habari Maelezo Bi. Zamaradi Kawawa

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Richard
Kasuga (kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam kuhusu utekelezaji wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa njia ya
vocha msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016 ambapo vocha hizo
zitawanufaisha wakulima takriban milioni moja wa mazao ya mahindi na
mpunga. Katikati ni Mkurugenzi wa Mazao kutoka wizara hiyo Bw. Twahir
Nzalawahe na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Pembejeo Bw. Shenal Nyoni.

Baadhi ya waandishi wa habari
wakifuatilia mkutano wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Picha zote na Fatma Salum (Maelezo)
--
Na. Georgina Misama – MAELEZO
Wakulima wapatao milioni moja wameanza kunufaika na usambazaji
wa vocha za pembejeo za kilimo ambazo Serikali inazitolea ruzuku kwa
ajili ya wakulima katika mikoa 24 ya Tanzania bara (ukitoa mkoa wa Dar
es Salaam) ili zitumike kufidia gharama ya mbolea na mbegu bora kwa
mwaka 2015/2016.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika Bw. Richard Kasuga amesema kwamba pembejeo za kilimo zenye
thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 78 zitawanufaisha wakulima
wanaojishughulisha na kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga.
“Usambazaji wa vocha hizo umeshaanza, Serikali kwa kushirikiana
na makampuni 23 ya mbolea na 27 ya mbegu bora ya mahindi na mpunga
yanaendelea kutoa huduma ya usambazaji wa pembejeo katika mikoa husika”
amesema Bw Kasuga.
Bw. Kasuga amesema kwamba ili kuhakikisha mbolea na pembejeo
zinatumika ipasavyo, Serikali inatekeleza jukumu hilo kwa kugawa
majukumu kwa ngazi mbalimbali ikianza na Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika, Kamati ya Taifa ya Uendeshaji wa Utaratibu wa Vocha, Mikoa,
Wilaya, Kata mpaka Vijiji.
Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua Serikali inafanya
juhudi gani katika kudhibiti ubora wa pembejeo hizo, Kaimu Mkurugenzi,
Mamlaka ya udhibiti wa Ubora wa Mbolea Bw. Lazaro Kitandu amesema toka
kuundwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea tatizo la ubora
limepungua kwa kiasi kikubwa kwani mamlaka hiyo inasimamia zoezi zima la
utengenezwaji na usambazaji wa mbolea na pia wakulima wanapewa elimu ya
matumizi sahihi na namna bora ya kuhifadhi.
Aidha, Serikali imetoa rai kwa wakulima kutumia ruzuku
inayotolewa ili waweze kujikomboa kiuchumi kwa kuboresha kilimo, na
kuwasihi baadhi ya wakulima wanaouza vocha zao wasidanganyike kwa
kupokea hela na kuuza haki yao.
Serikali ilianzisha utaratibu wa matumizi ya vocha mwaka
2008/2009 ili kuboresha mfumo wa usambazaji mbejeo kwa wakulima.
Utaratibu huu umesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, hivyo
Taifa kufaidika na kujitosheleza kwa chakula